
MAMLAKA ya mawasiliano
nchini (TCRA) imetoa onyo pamoja na kuutaka uongozi wa Clouds TV kuomba radhi
Watanzania kupitia taarifa zake za habari ndani ya siku tano mfululizo kuanzia
leo,
Adhabu hiyo imetolewa leo na kamati ya Maudhui ya
TCRA, baada ya baadhi ya wananchi hususani watazamaji wa kipindi cha ‘Take One’
kilichorushwa 28 Juni mwaka huu ambacho kilidaiwa kueleza masuala ya mapenzi ya
jinsia moja (Ushoga), kulalamikiwa kwamba kilikiuka maadili ya taifa.
Wakati akisoma tamko la adhabu hiyo, Joseph
Mapunda, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo amesema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa
baada ya wajumbe wa kamati kutafakari maelezo ya utetezi yaliyotolewa na
uongozi waClouds TV.
“Tumetafakari kwa kina maelezo ya utetezi
yaliyotolewa na clouds tv kuhusu kipindi chake cha Take One kilichorushwa
hewani tarehe 28 June 2016 ambacho kilikiuka baadhi ya kanuni za maadili ya
utangazaji,” amesema Mapunda.
Ameongeza kuwa “kutokana na kipindi hicho kuwakwaza
pamoja na kuwasababishia usumbufu wananchi hususan watazamaji kwa kuwasilisha
mada inayozungumzia masuala ya mapenzi ya jinsia moja (ushoga), Clouds TV
inatakiwa kuwaomba radhi watanzania wote na watazamaji.”
Amesema taarifa ya kuomba radhi itoke siku tano
mfululizo katika taarifa zao za habari ya saa moja na nusu na ya saa tano usiku
kuanzia siku ya kusomwa hukumu, na kwamba uthibitisho wa taarifa hizo upelekwe
TCRA siku ya Jumatano tarehe 13 Julai 2016 kabla ya saa kumi jioni.
“ Hatua ya pili, Clouds Tv inatakiwa kurekebisha
mapungufu yaliyojitokeza na kuhakikisha inazingatia kanuni zote za utangazaji
nchini katika kutekeleza majukumu yake ya utangazaji,” amesema na kuongeza.
“Kamati inawaonya vikali Clouds tv kwa kukiuka
kanuni za huduma za utangazaji (maudhui) ya mwaka 2005, namba 5(b), 5(c), 5(d)
na 15(c) 16(2) uamuzi huu umetolewa leo, haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi
huu iko wazi ndani ya siku 30 tangu siku uamuzi unapotolewa.
Ruge Mutahaba, Mkurugenzi wa Clouds Media Group
amesema baada ya kutafakari tamko la adhabu atatoa msimamo wake kama wataka
rufaa au la.
“Tunaweza tukarudi nyuma na kusema tufanye kazi ya
kukata rufaa, kwa sababu tunaamini na mimi nina simamia msimamo wangu kwamba
tunapoambiwa tunalinda maadili ya kitaifa, kupinga jambo lolote baya ni kulinda
maadili ya kitaifa,” amesema na kuongeza.
“Sasa ukiambiwa kwamba ulipinga kwa namna ya
ulivyo pinga ni tofauti kidogo labda inaweza ikasaida kutengeneza mjadala
mkubwa wa kujiuliza maadili tunayotakiwa kuyalinda ni yapi.”
Mutahaba amesema “Lakini moja kati ya kitu
tunachokiona kina utofauti ni kuna baadhi ya mambo yamezungumzwa ambayo
sikumbuki kabisa kama yako kwenye kipindi, kwa hiyo sijui wamezitolea wapi.”
Amesema kuwa ushoga ni tatizo na kwamba lazima
alikemee na ataendelea kulikemea.
“Kwa ajili ya kosa la kutaja neno shoga katika
kipindi cha njia panda mwaka 2000, miaka minne iliyopita kwenye gazeti
tulivyosoma neno ushoga tukatozwa faini ya mil 5, haiwezekani miaka kumi na
sita inapita kutaja neno shoga kila siku mtu anapewa adhabu,” amesema
Chapisha Maoni