0

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na matamshi ya Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam yanayokiuka misingi ya utawala bora aliyoyatoa tarehe 25 Agosti, 2016 wakati wa kuaga miili ya askari Polisi watatu waliouawa Mbande, Mkoani Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Bahame Tom Nyanduga, leo (Agosti 26, 2016) Mhe. Makonda ametumiwa barua ya wito inayomtaka afike makao makuu ya Tume mtaa wa Luthuli, tarehe 30 Agosti, 2016 ili kujadili kile Tume ilichokiona kuwa ni kejeli kwa Tume pamoja na jumuiya yote ya watetezi wa haki za binadamu.

Aidha, Tume imeona kuwa maagizo aliyoyatoa Mkuu huyo wa Mkoa kwa Jeshi la Polisi hayana msingi wa kisheria na hayako ndani ya mamlaka ya Mkuu wa Mkoa.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia Kifungu cha 27(1) na (2) (a) vya Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura Na. 391 ya Sheria za Tanzania 2002, THBUB ina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wa mtu au taasisi yoyote kuhusiana na utendaji wa kazi zake zinapokiuka mipaka ya madaraka yake, ili kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji huo.

Imetolewa na:

(SIGNED)
Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

Agosti 26, 2016

Chapisha Maoni

 
Top