0
Majeruhi wa tetemeko la ardhi Kagera wakipatiwa huduma ya kwanza
Watu 13 wameripotiwa kufariki dunia mkoani Kagera katika Halmashauri za Bukoba vijijini na manispaa ya Bukoba jana alasiri baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi.


Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amesema pia watu zaidi ya 200 wamejeruhiwa katika tukio hilo ambako lilizusha taharuki kwa wananchi wengi wa mikoa ya Kagera na Mwanza.
Ollomi amesema mpaka sasa bado kikosi cha uokozi cha zimamoto na chama cha msalaba mwekundu, wanaendelea na zoezi la kuwatafuta watu waliofukiwa katika nyumba zilizoanguka kutokana na tetemeko hilo.
Hata hivyo, Kamanda Ollomi amesema ataendelea kutoa taarifa za tukio hilo pale atakapopata habari kutoka maeneo yalikoathirika na tetemeko hilo mkoani humo.
Naye Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, amethibitisha kutokea kwa tetemeko hilo mkoani mwanza, lakini hakuna madhara yoyote yaliyoripotiwa kutokana na janga hilo.
Nchi za jirani na Tanzania za Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya nazo pia zilikumbwa na kishindo cha tetemeko hilo.

Chapisha Maoni

 
Top