0
Nape Nnauye
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye ametoa ahadi ya kuwa bega kwa bega na kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys kuanzia kesho asubuhi huku mashabiki wakiingia bure katika mchezo wao dhidi ya Congo.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Waziri Nape amesema katika kuwaunga mkono yeye kama waziri mwenye dhamana, ameamua kuonyesha mfano kwa kuichagia timu hiyo na kuipa motisha huku akiahidi kutoa kitita cha pesa kwa kila mchezaji.
“Katika kuhamasisha watanzania kuichangia timu yetu, mimi waziri mwenye dhamana ya michezo, nitatoa shilingi laki 2 kwa kila mchezaji kesho asubuhi nitakapokunywa nao chai, lakini kwa kila goli litakalofungwa nitatoa laki 5 kwenye timu, kwa hiyo wakifunga magoli 10 wana milioni zao 5, nafanya hivi kuhamasisha watanzania wengine nao waguswe ni timu ya vijana inafanya vizuri, na tunaamini yapo matumaini”, alisema Waziri Nape.
Waziri Nape aliendelea kwa kuwataka watanzania kwa ujumla kuchangia na kuwekeza kwenye timu hiyo changa ili kuipa nguvu zaidi, kwani inaonesha kuwa na mafanikio hapo mbeleni kutokana na kuanza na vijana wadogo wenye uwezo mzuri.
“Lazima watanzania tuamue kuwekeza katika timu hii, tumeona tukiwekeza kwa vijana wadogo mambo yanakwenda vizuri, sasa tuwekeze kwa hawa, tuanzie hapa tuone mafanikio yake yatakuwaje, watanzania tuchagie kidogo ulichonacho, kitafanya hii timu kuwa fahari yetu”, amesema Waziri Nape Nnauye.
Kwa upande wa TFF, kupitia kwa afisa habari Alfred Lucas amesema maandalizi ya mchezo wa kesho ambao timu hiyo inatarajia kucheza, yameshakamilika, na wanachokisubiri kwa sasa ni kupulizwa kwa kipyenga cha mwamuzi aliyepewa jukumu la kusimamia sheria 17 za mchezo huo huku wakiwaita mashabiki kuiunga mkono timu yao.
Lucas pia amethibitisha kuwa viingilio katika mchezo huo vimeondolewa ili kutoa fursa kwa mashabiki kuujaza uwanja huo, kwa ajili ya kuwatia nguvu vijana wa Serengeti Boys
Naye kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana Serengeti Boys Bakari Shime amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mchezo huo, na anaamini maandalizi aliyoyafanya yatazaa matokeo chanya ambayo yataiweka timu yake katika mazingira mazuri kabla ya mchezo wa mkondo wa pili ambao utachezwa mjini Brazzaville baadaye mwezi huu.
“Tunafahamu tuna mechi ngumu dhidi ya Kongo na tunaheshimu Congo ni timu nzuri, na tumejiandaa kulingana na ubora ambao Kongo wamekuwa nao, mechi ya kesho kwa vyovyote vile ni timu mbili ambazo zimeweza kuvuka vikwazo vingi mpaka kufikia hapa, na zimekuwa na uzoefu mkubwa, naamini na wao wamejindaa, na yule ambaye ataweza kutumia vizuri nafasi ambazo wamezitengeneza, anaweza kuwa mshindi”, alisema Shime.

Chapisha Maoni

 
Top