0
Waziri Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia) akiwa katika kivuko cha Mv Tanga
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua kivuko kipya na cha kisasa cha Mv. Tanga kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni na kuzindua Gati ya Bandari ya Pangani wilayani pangani mkoani Tanga.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Mbarawa amesema kuwa ujio wa kivuko hicho utafungua fursa za kibiashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi wilayani hapo.
“Naamini ujio wa kivuko hiki utarahisisha huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi wilayani hapa, hivyo naomba mkitunze vizuri kivuko hiki ili kiweze kudumu kwa muda mrefu”, amesema Prof.Mbarawa.50 242
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha huduma za kivuko zinakuwepo muda wote wilayani hapo, serikali kupitia wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa boti ambayo itatumika kama mbadala wa usafiri wakati wa usiku katika maeneo hayo ambapo kivuko cha MV. Tanga hakifanyi kazi.
Kuhusu ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani Waziri Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa gati hiyo utapelekea Meli kubwa kuweza kutia nanga na kurahisisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Pangani kwenda visiwa vya Unguja na Pemba.
Amefafanua kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataanzisha huduma ya boti za haraka kutoka Pangani kwenda Mkokotoni Zanzibar hivyo kufungua fursa za kibiashara na kitalii baina ya Tanga na Zanzibar.
Kwa upande wa huduma za mawasiliano ya simu wilayani hapo, Prof. Mbarawa amesema kuwa huduma hiyo itaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa mkandarasi kufika na kuanza ujenzi wa miundombinu ya simu na hivyo kuondoa tatizo la mawasiliano wilayani hapo.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amehahidi kuanza ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo (KM 242) kwa kiwango cha lami ifikapo mwakani.
Amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa wa awamu ili kuweza kuharakisha kukamilika kwake ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha barabara ya Tanga- Pangani (KM 50) na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utafungua fursa za kiuchumi kati ya Tanga na Pangani.

Chapisha Maoni

 
Top