0
Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela.
Wilaya ya Iringa bado inakumbwa na changamoto kubwa ya mimba za utotoni kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela kwenye mahojiano maalum na East Africa Radio na kusema kuwa mimba hizo zinatokana na watoto kwenda shuleni kwa kutembea umbali mrefu na kurubuniwa pindi wawapo njiani na kesi nyingi zimekuwa zikifichwa na wazazi au walezi.
Amesema kutokana na tatizo hilo wameweka mpango maalum wa kuwachunguza wanafunzi mara kwa mara sambamba na kuwaelekeza maafisa maendeleo na ustawi wa jamii kuhakikisha wanawahoji wanafunzi na kuwachunguza kila baada ya muda fulani kupita.
Amesema changamoto wanazokutana nazo katika kuwasaka wanaowapa mimba wanafunzi hao ni wafanyabiashara ambao pindi wakigundua wanatafutwa na vyombo vya usalama hukimbia kwa lengo la kukwepa tatizo.
Amesema wameweka mkakati wa kuhakikisha watoto wanatembea umbali mfupi kwenda na kurudi shuleni, pia kuwashawishi watembee kwa vikundi ili walindane, sambamba na na kuwabaini wanaowasumbua watoto na kuwachukulia hatua zaidi za kisheria, na kuwataka walimu wawasimamie wanafunzi wanapokuwa mashuleni.
Amesema tayari wamewakamata baadhi ya wazazi ambao wanahusika na kesi za kuwabaka watoto wao na kuwataka wazazi wanaolea watoto wa kambo wawape matunzo sawa na sheria na haki ya watoto zinavyoelekeza.

Chapisha Maoni

 
Top