Klabu ya soka ya Rayol Sports imempoteza kocha wake msaidizi Hamad Ndikumana ambaye amefariki usiku wa kuamkia leo ambapo ripoti za awali zinasema kifo chake kimesababishwa na matatizo ya Moyo.
Kifo cha Ndikumana sio tu kitawaumiza viongozi wa klabu hiyo bali ni wapenda soka wote wa Rwanda na ukanda wote wa Afrika mashariki na kati kutokana na umahiri wa Ndikumana alioujenga tangu mwaka 1998 alipoanza kuitumikia klabu ya Rayol Sports.
Ndikumana ambaye alikuwa anacheza nafasi ya ulinzi wa pembeni akicheza pande zote kulia na kushoto alijizolea umaarufu kiasi cha mashabiki kumpachika jina la Kataut kutokana na uwezo wake wa kupokonya mpira washambuliaji (Tackling).
Uwezo wake ulionekana kuwa mkubwa zaidi kwenye soka akiwa na umri wa miaka 19 tu kiasi cha kuzivutia klabu mbalimbali za Ulaya. Kataut alifanikiwa kuzichezea timu za KV Turnhout na KV Mechelen za Ubelgiji kati ya miaka ya 2000 na 2003.
Baadae alijiunga na klabu ya RSC Anderlecht ya hukohuko Ubelgiji kabla ya kucheza klabu zingine kadhaa kwenye nchi mbalimbali barani Ulaya hadi mwaka 2011 alipomalizana rasmi na klabu ya soka ya APOP Kinyras Peyias FC ya Cyprus ambapo alirejea nyumbani Rwanda na kisha kujiunga na klabu ya Stand United ya Shinyanga ambapo hakudumu sana.
Rayol Sports ilibaki kuwa nyumbani kwa Kataut kutokana na upendo wa mashabiki wa klabu hiyo kwake tangu akiwa mdogo ambapo baada ya kustaafu kucheza soka aliibukia kwenye majukumu ya ukocha akiwa kocha msaidizi wa Rayol Sports chini. August 8 aliiongoza Rayol Sports dhidi ya Simba kwenye Tamasha la ‘Simba Day’ ambapo walipoteza kwa bao 1-0.
Kwaheri Ndikumana zaidi na zaidi Watanzania hawatakukumbuka kwa kuwa mchezaji pekee kwani kila mpenda soka na burudani alimfahamu Ndikumana kama mume wa mwigizaji Irene Uwoya ambao walifunga ndoa mwaka 2007 na kufanikiwa kupata mtoto mmoja ambaye ni Krish, lakini hadi anafariki walikuwa wametengena.
Chapisha Maoni