0

Upande wa Jamhuri katika kesi ya tuhuma za utakatishaji fedha inayowakabili waliokuwa vigogo wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu, umedai mahakamani kwamba bado haujapokea nyaraka kutoka kwa rais huyo.

Madai hayo yalitolewa na Wakili wa Serikali, Leonard Swai, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa jana  kwa ajili ya kutajwa lakini upelelezi bado haujakamilika na kwamba bado wanasubiri nyaraka kutoka kwa Aveva.

"Mheshimiwa Hakimu, upande wa Jamhuri bado hatujakabidhiwa nyaraka tulizoomba kutoka  ofisi ya Aveva ili wakamilishe upelelezi," alidai Swai.

Hata hivyo, upande wa utetezi alidai kuwa wameipokea barua ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (Takukuru) kuhusu maombi hayo na wanayafanyia kazi.

Hakimu Nongwa alisema kesi hiyo itatajwa  Januari 11, 2018 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Awali, upande wa Jamhuri  uliomba ufunguo kutoka kwa Aveva ili kuwawezesha kupata nyaraka hizo ikiwa ni sehemu ya kukamilisha upelelezi.

Katika kesi ya msingi, Aveva na makamu wake Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha dola za Marekani 300,000.

Washtakiwa hao wanadaiwa kula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya Machi 15,2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa  dola 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli. 

Chapisha Maoni

 
Top