Mahakama Kuu imekana kuitambua kampuni
ya Fosters Auctioneers and General Traders iliyohusika kuondoa vitu vya kampuni
za Freeman Mbowe kwenye jengo la Shirika la Taifa la Nyumba (NHC).
Hayo yalibainishwa jana na kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea Mbowe
ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, Peter Kibatala wakati wa usikilizwaji wa
maombi yaliyofunguliwa na mlalamikaji huyo kupitia kampuni ya Mbowe Hotels Ltd
dhidi ya NHC na kampuni hiyo ya udalali.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo jana, pamoja na mambo mengine Mbowe
aliiomba Mahakama iliamuru NHC na kampuni hiyo wamrejeshe katika jengo hilo
pamoja na vifaa na mali zake zinazoshikiliwa na kampuni hiyo.
Wakili Kibatala aliieleza Mahakama kuwa mteja wake aliondolewa katika jengo
hilo kinyume na sheria.
Alidai dalali aliyetumiwa na NHC kuziondoa kampuni za Mbowe katika jengo hilo
hajasajiliwa na Mahakama kwa kuwa walimwandikia Msajili wa Mahakama barua kujua
kama anatambulika, lakini alijibu kuwa haimtambui.
Kutokana na majibu ya msajilihuyo kupitia barua yake ambayo wameiwasilisha
mahakamani kama kielelezo, Kibatala alidai sheria na mchakato mzima uliotumika
vilikuwa ni batili.
Mawakili wa NHC, Ipilinga Panya na Aloyce Sekule walidai shirika hilo kabla ya
kumtimua Mbowe lilimwandikia notisi ya siku 30 iliyokwisha kisha akaongezewa
siku 30 zingine kama sheria inavyotaka ambazo ziliisha na kumpa tena siku 14,
lakini hakulipa deni.
Wakili wa kampuni ya Foster Auctioneers and General Traders, Aliko Mwamanenge
alidai madai ya kuwa mteja wake ni dalali wa Baraza la Usuluhishi na kwamba
anayesajiliwa kama dalali ni mtu binafsi na siyo kampuni, hayana ukweli kwani
upande wa mlalamikaji ulipoandika barua kuulizia uhalali wake ulipaswa kuuliza
jina la mmiliki kampuni hiyo.
Hata hivyo, wakili wa mlalamikaji Kibatala alidai notisi zinazodaiwa kuandikwa
na NHC zilipelekwa mahali pasipohusika kwa kampuni ya Free Media badala ya
Mbowe Hotels ambayo ina mkataba na NHC. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote,
Jaji Sivangilwa Mwangesi anayesikiliza kesi hiyo aliiahirisha hadi Oktoba 18,
mwaka huu atakapotoa uamuzi wa maombi hayo ya mlalamikaji.
Septemba Mosi, wafanyakazi wa kampuni ya udalali ya Foster Auctioneers and
General Traders walifika kwenye ofisi za kampuni ya Free Media na kuondoka
vifaa mbalimbali vya kazi, zikiwamo kompyuta na viti kwa madai kwamba mmiliki
wake, Mbowe anadaiwa na NHC fedha nyingi za kodi ya pango.
Chapisha Maoni