0
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kuahirisha mikutano na maandamano yake (UKUTA) yaliyokuwa ili kutoa nafasi kwa viongozi wa dini, serikali, vyombo vya dola na wadau kujadiliana kufikia muafaka.

Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ametangaza rasmi , kusitisha maandamano na mikutano ya siasa iliyokuwa ifanyike nchi nzima kuanzia kesho Septemba Mosi ili , kupisha nafasi ya viongozi wa dini kukutana na Rais Dkt. John Magufuli kutafuta suluhu ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Mbowe amesema CHADEMA imefikia uamuzi huo muhimu baada ya vikao na wito kutoka kwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja na asasi za kiraia.
“Viongozi wa dini na asasi za kiraia wametuomba, tusitishe maandamano hayo ili wapate nafasi ya wiki tatu mwezi huu kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ili kutafuta suluhu ya kisiasa na kama ikishindikana Oktoba Mosi maandamano hayo yataratibiwa upya” Amesema Mbowe
Mbowe amesema maamuzi hayo yanatokana na hali ya usalama kuwa tete, kukamatwa kwa viongozi na wanachama wake na pia mazoezi na vitisho vinavyoendelea kufanywa na majeshi mambo ambayo amedai yanaweza kusababisha umwagaji wa damu kwa raia wasiokuwa na hatia.
Amesema sababu ntingine ni kuendelea kufungiwa kwa vyombo vya habari ambavyo vinatangaza kuhusu oparesheni hiyo, ambapo amesema kuwa ndani ya mwezi mmoja kuna gazeti moja na vituo viwili vya Radio vimefungiwa.
Amelaani vitendo vya kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu, ambapo amesema hadi leo, inakadiriwa wanachama na viongozi wa CHADEMA zaidi ya 230 wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi.
Aidha Mbowe amewataka wanachadema na wafuasi wa chama hicho kuwa watulivu wakati wakisubiri viongozi wa dini kufanya mazungumzo hayo ili haki yao ya kikatiba iweze kupatikana.

Chapisha Maoni

 
Top