0
Zahanati ya Selela ya Wilayani Monduli
Wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Selela kata ya Selela wilaya ya Monduli mkoani Arusha wamelazimika kujifungua kwa kutumia tochi za simu pamoja na taa ya chemli kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme kwa takribani mwezi mmoja na wiki 2.

Mwana Mama Mwasiti Hemedy mkazi wa kijiji hicho amesema kuwa wamekuwa wakiwapeleka wajawazito kwenye zahanati hiyo kwa ajili ya kujifungua na kushuhudia wauguzi wakitumia tochi za simu kutoa huduma kwa wajawazito hivyo wameiomba serikali isaidie upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme ili waweze kupata huduma bora.
Mganga wa zahanati ya Selela Michael Msalu alikataa kuzungumzia suala hilo kwa kina kwa madai kuwa yeye si msemaji wa hilo lakini alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la kutumia simu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hao.
Akizungumzia suala hilo diwani wa kata ya hiyo Cathbet Meena, amesema kuwa licha ya zahanati hiyo kukosa umeme shughuli za kiuchumi na kijamii zimesimama katika kata hiyo ikiwemo biashara, mashine za kusaga nafaka kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili baada ya transfoma iliyowekwa na TANESCO kupata hitilafu.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa mkoa wa Arusha TANESCO ambaye ni Mhandisi mkuu Donasian Shamba amekiri kuwepo kwa tatizo hilo ambalo linasababishwa na masuala ya kitaalam yanayopelelekea transfoma kuungua mara kwa mara hivyo wametuma timu ya wataalam na mapema wiki hii kurekebisha tatizo hilo ili wananchi wapate huduma.
Wakazi wa selela wamelazimika kusimamisha shughuli zao za uchumi zinazotegemea nishati ya umeme hivyo wanaiomba serikali ichukue hatua ili waweze kurudi katika shughuli za uzalishaji zinazowaingizia kipato.
Diwani wa kata ya Selela Cathbet Meena

Chapisha Maoni

 
Top