Mabadiliko ya kidijitali yamekuwa moja ya chachu kubwa ya kusukuma mbele gurudumu la maendeleo nchini.
Juma lililopita, Umoja wa Forodha Ulimwenguni (WCO) uliweka bayana kwamba Tanzania inaweza kunufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuwekeza katika teknolojia.Akizungumza jijini Dar Es Salaam, Katibu Mkuu wa WCO amesema mbali na faida nyingi, uwekezaji katika teknolojia ya kidijitali ni mojawapo ya njia bora ya kukusanya kodi na mapato ya serikali, hivyo kuwezesha utoaji bora wa huduma nyingine ambazo zinategemea kodi hizo kama vile ujenzi wa miundombinu.
Mpaka hivi sasa, teknolojia ya kidijitali tayari imeleta matunda mazuri kwa Watanzania wengi na ipo mifano mingi. Kutuma na kupokea pesa kwa njia ya simu kwa mfano imesaidia kuwapa huduma rasmi ya kifedha (akaunti ya fedha kwenye simu) watu wengi ambao awali haikuwezekana hadi uwe na akaunti benki. Sote tunakumbuka miaka ya nyumba kidogo ambapo kila malipo ya serikali au kutuma fedha ilibidi benki lakini sasa unafanya popote ulipo na muda wowote kwa njia ya simu.Mtandao wa intaneti nao umebadili maisha ya wengi kwani umesaidia watu kuwasiliana vizuri zaidi na kwa gharama bora zaidi, na hata kusaidia biashara kuanza na kukua.
Ama kwa hakika, uwepo wa uwekezaji na huduma hizi toka sekta ya mawasiliano ya simu umesaidia kuinua sana maisha ya Watanzania. Huku sekta hii ikiendelea kupanuka, tayari imetoa ajira zaidi ya milioni moja na nusu, zisizo za moja kwa moja kwenye maeneo kama wahandisi wa teknolojia, wasambazi wa huduma na mawakala wa fedha. Kazi hizi zinasaidia mamilioni ya Watanzania kuwa na ajira na kipato cha uhakika na hivyo kuchangia kwenye uchumi wa nchi yao. Maana yake tunaweza kusema bila kusita kwamba mchango wa sekta hii ni mkubwa na muhimu katika uchumi wa Tanzania.
Umuhimu wa sekta hii ya mawasiliano ya simu za mkononi unatukumbusha kuendelea kuunga mkono ukuaji wa sekta hii kisera, kimfumo na kimazingira ya uwekezaji. Hii itasaidia na kuhakikisha sekta hii inabaki kuwa imara, inakua zaidi na sote tunaendelea kunufaika na faida zake.
Chapisha Maoni